Mgogoro mkubwa umeibuka ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Monduli kuhusu benki ipi itoe huduma za kibenki kwake kati ya benki mbili kubwa nchini za NMB na CRDB ambazo zote zimeshinda zabuni ya kutunza fedha za serikali na taasisi zake.
Taarifa zilizofikia Tazama Line mwishoni mwa wiki zinaeleza kuwa mgogoro huo umesababisha wajumbe wa Kamati ya Fedha na Uchumi wa Halmashauri ya hiyo kukabana mashati na kurushiana matusi ya nguoni wakati wakijadili ajenda ya kuchagua benki itakayotoa huduma za kibenki kwake.
Tukio hilo la kufedhehesha limetokea Mei 20 mwaka huu wakati wajumbe wa kamati hiyo nyeti ya halmashauri wakijadili ajenda hiyo, baada ya kupokea maelekezo kutoka Hazina kuhusu uamuzi wa serikali kuchagua benki mbili za CRDB na NMB kuwa ndizo zimeshinda zabuni ya kuhifadhi fedha za serikali na taasisi zake.
Taarifa zilizofikia gazeti hili kutoka ndani ya kikao hicho zinadai kuwa baada ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Edward Sapunyu, kufungua kikao mjadala kuhusu ajenda hiyo ulianza kwa wajumbe kupitia ushauri uliotolewa na wataalamu wa halmashauri.
Mvutano huo ndani ya kikao ulianza baada ya Mwenyekiti kuwasilisha hoja kuwa akaunti zote za halmashauri hiyo kuanzia sasa zihamishiwe kwenda benki ya CRDB haraka iwezekanavyo kutoka NMB jambo ambalo wajumbe wengine walilipinga.
Awali kabla ya agizo hilo la Hazina, Halmashauri ya Wilaya ya Monduli ilikuwa inahudumiwa na benki ya NMB, ambayo pia ina tawi katika mji wa Monduli kwa muda mrefu na ni kati ya benki hizo mbili zilizoshinda zabuni ya kutunza fedha za serikali na taasisi zake.
Barua ya Hazina:
Barua kutoka hazina kwenda kwa Mkurugenzi wa Wilaya ya Monduli ilifafanua kuwa serikali imeridhia na kuingia mkataba na benki mbili za NMB na CRDB kwa ajili ya kutoa huduma za kibenki kwa taasisi zake.
Barua hiyo ambayo Tazama Line limefanikiwa kuona nakala yake ya Mei 13 mwaka huu, ikiwa na kumbukumbu namba IE/031/2014-15/HQ/NC01/13 ikiwa na kichwa cha habari “MIKATABA YA UTOAJI HUDUMA ZA KIBENKI SERIKALINI”.
Barua hiyo imeandikwa kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Hazina na ofisa anayejitambulisha kwa jina la Aziz Kefile ambaye hata hivyo hakuisaini kwa taratibu zinavyoelekeza.
Katika barua yake, Kefile anamwelekeza Mkurugenzi huyo wa Halmashauri kuwa wanatakiwa kuchagua benki moja kati ya hizo mbili ili itoe huduma ya kibenki kwa halmashauri hiyo.
Barua hiyo inasomeka:”Kama tulivyoeleza katika barua yetu ya awali ulipaswa kuwasilisha kwa Mhasibu Mkuu wa serikali, jina la benki moja tu itakayotoa huduma za kifedha kwa halmashauri yako.
“Katika barua yako umetaja benki mbili za NMB Plc na CRDB kuwa zitatoa huduma kwenye ofisi yako. Mapendekezo yako hayakuzingatia maelekezo niliyoyatoa. Unashauriwa kuchagua benki moja tu ambayo itahudumia ofisi yako”iliendelea barua hiyo.
Mapendekezo ya wataalamu:
Katika mapendekezo yao, wataalamu wa halmashauri hiyo baada ya kujadiliana kwa muda mrefu walipendekeza kuwa akaunti za halmashauri hiyo ziendelee kuwa katika benki ya NMB Plc kwa sasa kutokana na changamoto ya CRDB kutokuwa na tawi kwa sasa wilayani Monduli.
Wataalamu hao wamedokeza kuwa halmashauri hyo inamiliki akaunti saba katika benki ya NMB ambazo ni pamoja na akaunti ya Mdc Own Source, Mdc Emolment, Mdc other Charges, Mdc Development, Mdc Deposit, Mdc Road Fund na Mdc Water Sector Accounts.
Chanzo cha mvutano:
Chanzo cha mvutano huo baina ya wajumbe wa kamati hiyo hadi kupelekea “kukwidana mashati” imelelezwa kuwa ni hatua ya Mwenyekiti Sapunyu kuwasili kikaoni akiwa tayari na barua mbili mkononi kutoka Halmashauri za Kinondoni na Ilala za jijini Dar es Salaam ambazo zinadaiwa kuwa zimeshahamisha akaunti zake kwenda CRDB.
Wajumbe wawili katika kikao hicho Julius Kalanga na Isaack Joseph “Kadogoo” walianza kuhoji sababu za Mwenyekiti huyo kushinikiza akaunti zote za halmashauri kuhamishwa kwa wakati mmoja kutoka benki ya NMB Plc kwenda CRDB bila hata ya kufanyika kwa tathmini na vigezo muhimu vya utoaji huduma.
Mmoja wa wajumbe wa kikao hicho aliyeomba jina lake lihifadhiwe aliiambia Raia Mwema kuwa wajumbe hao wawili waligeuka kuwa “mwiba” na kumtuhumu Mwenyekiti wa Halmashauri kuwa ana maslahi binafsi katika suala hilo na kutaka ushauri ulitolewa na wataalamu wa halmashauri uzingatiwe.
Mjumbe huyo alieleza kuwa hoja za wajumbe hao wawili ni kwamba kwanza benki ya CRDB inayopigiwa debe na Mwenyekiti wa Halmashauri haina tawi katika mji wa Monduli na huduma zake za kifedha zinapatikana katika mji wa Arusha umbali wa kilometa 45 kutoka Monduli.
“Hawa CRDB wana “kijitawi” katika eneo la sokoni mjini Monduli, na hakikidhi mahitaji ya utoaji huduma za kifedha kwa taasisi kubwa kama Halmashauri ya Wilaya Monduli ambayo ina shughuli nyingi za kuingiza na kutoa fedha,”alieleza mjumbe huyo.
Wajumbe hao pia walipinga sababu za Mwenyekiti kufuatilia barua hizo hadi halmashauri za wilaya za Ilala na Kindondoni wakati yeye si mtumishi wala mtendaji wa halmashauri.
“Wajumbe walihoji Mwenyekiti ana maslahi gani katika suala hili. Ni kwanini asisubiri na asizingatie ushauri wa wataalamu ambao wamependekeza suala hilo lipewe muda zaidi, kwa kuwa Monduli kama ilivyo kwa Halmashauri zote nchini inaendeshwa kwa kanuni na sheria,”alisema mjumbe huyo.
Mjumbe huyo aliongeza kuwa hoja nyingine ya wajumbe waliokuwa wanapinga uhamishaji wa akaunti hizo ni kwamba, uamuzi huo ungewaathiri watumishi wa Halmashauri ambao wengi akaunti zao za mishahara ziko benki ya NMB hivyo wangelazimika kusubiri siku tatu hadi nne kupata mishahara yao.
“Kwa mfano ukimlipa posho ya shilingi 75,000 mtumishi anayeishi katika kituo chake cha kazi kilomita 100 kutoka Monduli atalazimika kusubiri siku tatu mjini hapa ili hundi yake itoke CRDB na kuingia NMB hivyo kuingia gharama zisizo za lazima kama malazi,chakula na nyinginezo,”aliongeza.
Kwa mujibu wa mjumbe huyo mmoja wajumbe, Isaack Joseph alionya kuwa wao kama madiwani wamebakiwa na miezi mwili tu kumaliza muda wao kabla ya uchaguzi mkuu hivyo wasifanye maamuzi ambayo yatawaumiza,watumishi na wadau wengine wa halmashauri hiyo wasio na hatia.
Akimkakariri mjumbe huyo alisema:”Mheshimiwa Mwenyekiti sisi kama viongozi wa kuchaguliwa muda wetu umeisha, hatuna uhakika kama tutachaguliwa tena kuwa viongozi hivyo maamuzi haya yasije yakageuka kuwa “maumivu” kwa watumishi wa halmashauri na wadau wengine kwa ushauri wangu ingekuwa vyema tukajipa muda hadi CRDB wafungue tawi hapa halafu tuoanishe huduma zao pamoja na za NMB Plc”.
Hata hivyo Mwenyekiti anaelezwa kupuuza hoja hizo na kutaka wajumbe wapige kura hatua ambayo ilisababisha majibizano makali yaliyopelekea wajumbe kupandisha “mori” kukabana mashati ambao wataaalmu wa halmashauri wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Godfrey Luguma waliingilia kati na kuwatengenisha.
“Hali ilikuwa mbaya, baada ya Mwenyekiti kuona anazidiwa hoja aliamuru kura zipigwe hatua ambayo wajumbe walipinga kwa maelezo kuwa kanuni za halmashauri haziruhusu, hatua iliyomlazimisha Mwenyekiti kuahirisha kikao huku wakirushiana matusi ya nguoni,”aliongeza mtoa taarifa wetu.
Kauli za wahusika:
Akizungumza na Raia Mwema juzi Jumatatu, mmoja wa wajumbe wa kikao hicho anayepinga akaunti za halmashauri kuhamishwa, Isaack Joseph, hakutaka kukanusha wala kukubali kutokea kwa vurugu katika kikao hicho.
“Kwanza sielewi umepata wapi taarifa hizo, ila nataka nikuambie kuwa vikao vya halmashauri vinaongozwa na kanuni hivyo yote yaliyozungumzwa na kuazimiwa yako katika muhtasari naomba uwasiliane na Mkurugenzi wa Halmashauri anaweza kukueleza vizuri,”alisema mjumbe huyo.
Kwa upande wake mjumbe Kalanga hakuweza kupatikana kutokana na simu yake kuita kila alipogiwa bila ya kupokewa.
Hata hivyo Luguma alikiri kutokea kwa malumbano baina ya wajumbe na kufafanua kuwa “yalikuwa na maslahi makubwa kwa halmashauri ya wilaya hiyo”.
“Kulikuwa na majadiliano katika kikao ambayo kwa namna moja au nyingine yalikuwa ni kwa maslahi mapana ya halmashauri yetu, ila taarifa za wajumbe kukabana koo na kutukanana hazina ukweli wowote,”alisema.
Aliongeza kuwa pamoja na kutokea malumbano hayo anaamini kuwa suala hilo litafikia muafaka kwa dosari ndogondogo kurekebishwa na kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Kwa upande wake, Sapunyu hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa maelezo kuwa “ukurasa wake” umefungwa na akaunti hizo zitahamishwa.
“Wajumbe wote wamesharidhia kuwa akaunti zihamishwe, hivyo mjadala huo umefungwa siwezi kuzungumza na mwandishi zaidi ya hapo,”alisema Mwenyekiti huyo wa Halmashauri.
CRDB wajibu:
Juhudi za kumpata Msema wa NMB Plc hazikuweza kufanikiwa, lakini akizungumza na gazeti hili Msemaji wa CRDB, Tully Mwambapa, alifafanua kuwa katika kipindi hiki chenye ushindani mkubwa wa kibiashara katika sekta ya fedha “alitarajia malalamiko ya aina hiyo”.
“Kwanza ieleweke kuwa katika kutafuta masoko ni lazima ufanye ushawishi, na hilo halijafanyika Monduli pekee bali halmashauri zote nchini hivyo watu wasitake kuturushia mawe wakati wao pia wanaishi katika nyumba za vioo,”alisema Mwambapa bila ya kufafanua zaidi.
Alisema ili kuboresha huduma zake katika maeneo yote nyeti nchini, benki hiyo imeanzisha mpango maalumu wa utoaji huduma kwa njia ya kisasa zaidi kwa kutumia mifumo ya kompyuta na kuwa taasisi ya kwanza ya fedha kuwa na huduma hizo.
“Naomba niwatoe hofu wanaolalamika kuwa uhamishaji wa fedha kwa mfano mishahara ya watumishi inaweza kuchukua muda mrefu kwa kuanzisha huduma ya service centre katika halmashauri zote na kwamba suala hilo lilishapatiwa ufumbuzi na sasa mtumishi anaweza kupata mshahara wake ndani ya saa 24,”aliongeza.
Alitaja huduma zinazorahisisha uhamishaji wa fedha kutoka akaunti moja kwenda nyingine ni pamoja na Fahari Huduma Wakala, Ubia na Shirika la Posta nchini, Simu Banking na Services Centre hivyo kuwa na uwezo wa kutoa huduma za kibenki kutoka eneo lolote la nchi bila ya kujali changamoto za kijiografia.
Powerd by Raia Mwema.
Siku zote bahati yako iko mikononi mwako tu, ili kudhibitisha kuwa ni kweli bofya kwenye picha iliyopo hapa chini.
Post a Comment