Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad amesema ilikuwa kazi kubwa kumshawishi Juma Duni Haji kukiacha chama hicho na kujiunga Chadema ili awe mgombea mwenza wa Edward Lowassa.
Duni, ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF, alitangazwa kujiunga
na Chadema jana, ikiwa ni makubaliano ya mkakati maalumu wa vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wa kukabiliana na
kikwazo cha kisheria cha kupata mgombea mwenza kutoka chama tofauti na
kilichosimamisha mgombea urais.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inataka Makamu wa Rais
kutoka chama kilichoshinda kiti cha urais na hivyo Duni amejiunga na
Chadema akiwa mwakilishi wa Ukawa kwenye Serikali iwapo umoja huo,
unaoundwa na CHADEMA, CUF, NLD na NCCR – Mageuzi utashinda Uchaguzi Mkuu.
“Tulimwita Babu Duni, tukamwambia azma hii, akasema; ‘hivi kweli niende Chadema mie?’”
alisema Maalim Seif akimnukuu Duni wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa
Chadema jana kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.


“Nikamwambia kwa hili tunalotaka la mabadiliko, lazima uende Chadema.”
Maalim Seif, ambaye alikuwa mmoja wa wageni waalikwa waliopewa nafasi
ya kuzungumza kwenye mkutano huo ambao ni chombo cha juu cha uamuzi cha
Chadema, alisema kikubwa kinachotakiwa ni kuunganisha nguvu kuhakikisha
kuwa upinzani unatwaa Dola katika uchaguzi ujao wa Rais, wabunge na
madiwani.
Maalim Seif, ambaye alijitangazia ushindi wa kiti cha urais wa
Zanzibar, pia alimtangaza Lowassa, ambaye pia aliondoka CCM na kujiunga
na Chadema wiki iliyopita, kuwa ameshashinda mbio za urais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania pamoja na mgombea mwenza na wanachosubiri sasa ni
kuapishwa tu.
“Huu ni wakati wa kujiamini na kuamini kuwa tunaweza kuchukua dola,” alisema
Maalim Seif ambaye pamoja na mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba
waliiongoza CUF katika kupatikana kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya
Zanzibar (SUK).
Wakati Maalim Seif akitangaza ushindi kwa Ukawa, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alionya kuwa kazi ya kuiondoa CCM si rahisi na kwamba nguvu ya Watanzania inahitajika kufanikisha azma hiyo.
Post a Comment