Dodoma. Jumla ya Sh600 bilioni zitatumika katika Mradi wa Kuendeleza Jiji la Dar es Salaam (DMDP), katika mwaka wa fedha 2015/2016, ikiwamo kuboresha miundombinu ili kudhibiti mafuriko.
Waziri wa Nchi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia alisema hayo bungeni jana aliposoma maelezo kuhusu mapitio ya kazi ya wizara yake kwa mwaka huo wa fedha. “Mradi wa DMDP, utatekelezwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia (WB),” alisema Waziri Ghasia.
Alisema kazi zilizopangwa kwenye mradi huo ni kuimarisha miundombinu ya barabara za mabasi yaendayo haraka. Waziri Ghasia alisema fedha hizo zitatumika kujenga mifereji mikubwa na midogo ya maji ya mvua katika maeneo yanayoathiriwa na mafuriko mara kwa mara hasa mabondeni.
Alisema mradi huo umegawanyika katika sehemu tatu, ya kwanza ni kuboresha miundombinu ya barabara na mifumo ya maji ya mvua katika mabonde matano yaliyopo katika halmashauri za Manispaa ya Jiji la Dar es Salaam.
Alisema sehemu ya pili ya mradi huo itaboresha njia za waenda kwa miguu, taa za barabarani, madaraja pamoja na miradi ya ujenzi inayohusiana na usafi wa mazingira. Waziri Ghasia alisema sehemu ya tatu ya mradi huo, itazijengea uwezo taasisi zinazotoa huduma kwa jamii.
Hata hivyo, alisema ili mradi huo utekelezwe, Serikali inapaswa kulipa fidia kwa wananchi wote watakaoathirika kutokana na utekelezaji wake.“Dola 23.4 milioni za Marekani, zitatumika kwa ajili ya kulipa fidia. Manispaa zote za Mkoa wa Dar es Salaam zimeshatenga fedha katika bajeti zao,” alisema Waziri Ghasia.
Alisema katika kuanza utekelezaji wa mradi huo kwa mwaka wa fedha wa 2015/16, Sh11.7 bilioni zitatumika katika shughuli za ujenzi wa barabara.
“Sh5.6 bilioni zitatumika kwa ajili ya usimamizi wa shughuli za miradi,” alisema Waziri Ghasia.
Hivi sasa katika Jiji la Dar es Salaam, miundombinu mbalimbali imeharibika kutokana na mvua zinazoendelea.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mhandisi Mussa Natty alisema juzi kuwa Daraja la Mdidimua - Msakuzi, Mtaa wa Luguruni, Kata ya Kwembe lilibomoka kutokana na mvua hizo.
Alisema daraja kati ya Mtaa wa Jongo na Mianzini linahitaji kuondolewa udongo ili maji yapite kirahisi.
Post a Comment