Rais Jakaya Kikwete amewataka Watanzania
kufanya kampeni za kistaarabu, kwakuwa nchi ya Tanzania inayo sifa ya
kuendesha mambo yake kwa njia ya amani na utulivu.
Alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati
akihutubia mamia ya wakazi kwenye hafla maalumu ya kuwaaga wananchi wa
mkoa wa Tanga, iliyofanyika katika uwanja wa Mkwakwani jijini hapa.
Katika hafla hiyo, ambayo Rais Kikwete
aliongozana na Mama Salma Kikwete alipata fursa ya kupokea zawadi za
aina mbalimbali kutoka kwa wawakilishi wa wananchi kutoka wilaya za
Tanga, Mkinga, Pangani, Muheza, Korogwe, Lushoto, Handeni na Kilindi
ambazo zinaunda mkoa huo.
Alisema kwa kuwa kampeni za Uchaguzi
Mkuu utakaofanyika mwezi wa Oktoba zitaanza rasmi Agosti 21 mwaka huu ni
vyema wananchi kila mmoja kwa nafasi yake, wahakikishe zinafanyika kwa
ustaarabu na utulivu ili kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo
nchini.
“Tanzania
ina sifa ya kuendesha vitu kwa amani na utulivu …naomba kampeni
zitakazofanyika za kuwanadi wagombea wa udiwani, ubunge na urais ziwe za
kistaarabu hakuna sababu ya kufanya vurugu bali kila mtu apewe nafasi
ya kumwaga sera zake, asikilizwe kwa utulivu”, alisema.
Aidha, Rais Kikwete aliwashukuru wakazi
wa Tanga kwa kuiunga mkono CCM sambamba na kumuunga mkono kwa kiwango
kikubwa kwenye chaguzi zote, zilizomuweka madarakani mwaka 2005 na 2010,
ikilinganishwa na baadhi ya mikoa mingine nchini.
“Wito
wangu kwenu ichagueni CCM tu katika serikali inayokuja, chama hiki
kitawajengea Chuo Kikuu cha Serikali kwa sababu hapa Tanga hamna… naomba
wananchi tujiandae vizuri kwa ajili ya kushiriki uchaguzi huo mkuu,” alisema.
Awali, akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Magalula Saidi Magalula alisema “Wananchi
wa mkoa huu wameniagiza niwasilishe kwako maombi ya vitu vifuatavyo
ujenzi wa daraja la Mligazi linalounganisha wilaya ya Handeni na Miono,
pia ujenzi wa barabara ya Tanga- Pangani–Bagamoyo kwa kiwango cha lami,
Bandari ya Tanga, kufufuliwa kwa viwanda mbalimbali vya uzalishaji na
kufufuliwa kwa reli ya Tanga – Moshi hadi Musoma”.
Siku zote bahati yako iko mikononi mwako tu, ili kudhibitisha kuwa ni kweli bofya kwenye picha iliyopo hapa chini.
Post a Comment