Wanajeshi wa Uganda wakishirikiana na maafisa wa polisi wamevamia na kuzingira afisi za chama cha upinzani za Forum for Democratic Change (FDC).
Kiongozi wa chama hicho, Dkt Kizza Besigye, ambaye amekuwa akiwania urais amekuwemo ndani ya afisi hizo na mwandishi wa BBC Patience Atuhaire anasema polisi wameondoka naye akiwa kwenye gari lao.
Kituo cha televisheni cha NBS kimeripoti kuwa Besigye na rais wa FDC Mugisha Muntu wamekamatwa katika makao makuu hayo eneo la Najjanankumbi, na wafuasi wa chama hicho wakatawanywa kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi.
Mgombea mwingine wa urais Amama Mbabazi amepakia video kwenye Twitter inayoonesha maafisa wa usalama nje ya nyumba yake.
Anasema polisi wameanza kuwakamata watu nje ya nyumba yake.
Viongozi wa chama cha FDC walikuwa wakijiandaa kuhutubia wanahabari kuhusu uchaguzi mkuu uliofanyika jana.
Maafisa wa usalama wanashika doria kwa wingi maeneo yanayozunguka makao makuu hayo ya chama cha FDC, mwandishi wa BBC Catherine Byaruhanga anasema.
Milio inasikika ingawa haijabainika iwapo ni ya risasi halisi, risasi za mipira au mabomu ya kutoa machozi.
Post a Comment