Serikali yasitisha mkataba wa mkurugenzi wa bodi ya mikopo na kusimamisha kazi wakurugenzi 3.
Waziri wa elimu, sayansi, teknolojia na mafunzo ya ufundi, Prof Joyce Ndalichako amesitisha mkataba wa mkurugenzi wa bodi ya mikopo na wakurugenzi wengine wa tatu kutokana na utendaji mbovu katika kuendesha bodi hiyo uliosababisha upotevu wa zaidi ya sh bilioni tatu.
Akitangaza uamuzi huo jijini Dar es Salaam Prof Ndalichako mbali na kuwataja waliosimamishwa pia amemwagiza mkaguzi wa ndani mkuu wa serikali kufanya ukaguzi maalum kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2013 hadi sasa.
Aidha amesema wizara yake imefikia uamuzi huo baada ya kuridhishwa na ukaguzi uliofanywa na mkaguzi wa ndani mwaka 2009 hadi 2013 na kubaini madhaifu kadhaa ikiwemo mikopo kupitia vyuo viwili tofauti, wasiokuwa na usajili, walioacha masomo, mikopo kutolewa bila kupitishwa na kamati ya mikopo, kupewa mikopo bila kuomba na wengine waliokuwa wanasoma nje ya nchi kulipiwa mikopo miaka saba badala ya minne.
Hata hivyo amevionya vyuo vyote nchini ambavyo kwa namna moja au nyingine vimekuwa vikishirikiana na bodi hiyo kufanya udanganyifu na vitakavyobainika serikali itachukuwa hatua kali na kwamba kutokana na nafasi hizo kuwa wazi serikali itateua maafisa watakaoshika nafasi hizo kwa mudahadi uchunguzi utakapokamilika.
Wakati hayo yakitokea katika wizara ya elimu naye naibu waziri wa Tamisemi Mh Suleiman Jaffo amemwagiza meneja wa shirika la masoko Kariakoo kuandika barua ya kujieleza kwa nini hajaanza kutumia mfumo wa elektroniki wakati waziri mkuu alishaagiza hadi kufikia januari 10 wawe wamehamia kwenye mfumo huo hali inayochangia serikali kutokupata mapato yanayostahili.
Post a Comment