Uongozi wa Bandari ya Tanga wapewa siku 16 kutoa taarifa juu ya ununuzi wa Matishari.
Waziri mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa ametoa masaa 16 kwa uongozi wa mamlaka ya usimamizi wa bandari tawi la Tanga kumpa taarifa kamili iliyosababisha kununua matishari manne yenye thamani ya zaidi dola milioni 10.1 kutoka nchini China wakati mahitaji ni matishari mawili.
Akizungumza baada ya ukaguzi wa matishari na vitendea kazi vingine katika bandari hiyo, waziri mkuu amesema serikali ilikuwa na lengo la kupunguza usumbufu na gharama kwa wateja wa bandari hiyo ambapo alimtaka mhandisi wa bandari Bwana Felix Mtui kutoa majibu ya papo kwa papo ili kuleta uwiano wa kile atakachoulizwa na majibu yake.
Hata hivyo waziri mkuu alipombana kaimu meneja wa bandari tawi la Tanga Bwana Henry Arika kuelezea utaratibu wa kuchukua mafundi kutoka nchi jirani ya Kenya kwa ajili ya kurekebisha miundo mbinu ya matishari hayo na gharama zake zikoje meneja huyo alikwepa na kudai kuwa yeye ni mgeni na amekuja miezi kadhaa kukaimu nafasi hiyo.
Katika ukaguzi huo waziri mkuu aliwaagiza maofisa wa mamlaka ya mapato nchini tawi la Tanga, uongozi wa mamlaka ya bandari kwa kushirikiana na jeshi la polisi kuhakikisha wanadhibiti uingizaji wa sukari kutoka Brazil ambayo imekuwa ikiingizwa nchini kinyume cha sheria bila kulipiwa ushuru na kufanyiwa ukaguzi na mamlaka ya chakula na dawa nchini TFDA hatua ambayo imekuwa ikiathiri soko la ndani.
Post a Comment