Baadhi ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliomuunga mkono Waziri Mkuu msfaaru, Edward Lowassa, katika mbio zake za kuomba uteuzi wa kugombea urais kabla ya kukihama chama hicho, wamefunguka.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara, Christopher Sanya, amesema kitendo cha Lowassa, kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinaashiria chama hicho kumomonyoka, baada ya kumalizika kwa kura za maoni.
Alisema ni pigo kubwa kwa CCM na litasababisha madhara makubwa baada ya kura za maoni kumalizika.
“Lowassa ametumia haki yake kufanya hivyo, kama mwenyewe alivyosema hakuridhishwa na mchakato mzima wa kumpata mgombea urais wa CCM ingawa ni pigo kubwa kwa chama chetu,” alisema Sanya na kuongeza kuwa uamuzi wake sio wa kubeza kwani yeye ni mtu kukatwa Dodoma alikaa kimya muda mrefu bila kuzungumza chochote hadi alipofikia kuchukua maamuzi hayo ya juzi.
Mbunge wa Mwibara anayemaliza muda wake, Kangi Lugola, alisema uamuzi huo una madhara makubwa kwa CCM hasa kipindi hiki.
“Kwanza namtakia kila la heri katika kuendeleza safari yake ya matumaini, huyu ni mtu mzima, mwenye elimu, amekuwa kiongozi mwandamizi serikalini na mkongwe wa siasa, hivyo hadi kufikia hatua hiyo hakufanya maamuzi ya pupa bali ametumia busara na hekima kubwa,” Lugola.
Hata hivyo, alipoulizwa endapo atamuunga mkono kwa kuhamia Chadema, alisema anatambua kufanyiwa mizengwe mingi na viongozi wa CCM ngazi ya wilaya, lakini kwa sasa anashiriki katika kura za maoni akiamini viongozi hawawezi kumzuia kuingia bungeni kwa mara nyingine.
“Nilienda Dodoma miaka mitano hii tunayomaliza kwa kupelekwa na wananchi wa Mwibara, wananchi hao hao bado wapo hivyo viongozi wa CCM watambue pia nitapelekwa Bungeni na wananchi hao hao si viongozi wa chama,” Lugola.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Hamisi Mgeja, alisema licha ya Lowassa kuwekeza jasho lake kwa kipindi kirefu ndani ya CCM, lakini ana haki na ni mtu mzima ambaye hawezi kuingiliwa katika kufikiwa maamuzi yake.
“Ingawa hili ni jambo kubwa na zito, lakini tumekuwa naye kwa kazi, tumeshirikiana naye kukijenga chama chetu, lakini ikifika mahali huwezi kuzuia mtu kufanya maamuzi yake,” Mgeja.
Hata hivyo, alisema licha ya rafiki yake kuondoka, yeye atabaki kuwa mwana-CCM mwaminifu na muadilifu na mwenyekiti wa mkoa huo.
Mwanasiasa Mkongwe na kada maarufu wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru, alisema: “Kwa sasa sina cha kusema, bwana mwandishi, no comment, ila nitatoa comment zangu wakati muafaka utakapowadia.”
Naye Mwenyekiti wa CCM, mkoa wa Singida, Mgana Msindai, alisema kwa sasa hana maoni na kuomba apatiwe muda hadi leo.
Mbunge wa Ilala, Mussa Azan Zungu, alisema hana maoni na anasuburi chama kitoe maamuzi yake.

NIPASHE
Klabu ya soka ya Azam ya Tanzania Bara imeanza mazungumzo rasmi ya kumsajili mshambuliaji hatari wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya, Gor Mahia, Michael Olunga, na imeelezwa jana jijini Dar es Salaam kwamba wako tayari kulipa Dola za Marekani 300,000 (Sh. milioni 600) ambazo wametajiwa.
Wakurugenzi na kocha mkuu wa Kituo cha Liberty cha jijini Nairobi, Kenya, Jacob Mulee ‘Ghost’, alisema kuwa viongozi wa Azam wamemfuata rasmi kwa ajili ya kumsajili Olunga na wameonyesha nia ya kumuhitaji kwenye timu yao.
Ghost ambaye aliwahi kuipa ubingwa wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) 2008 jijini Dar es Salaam, alisema kuwa kwanza viongozi wa klabu hiyo walianzia dau la Dola za Marekani 30,000 lakini aliwaeleza kuwa kiasi hicho cha fedha ni ‘dharau’ na hakifanani na kiwango cha mchezaji huyo.
“Nimeongea na (alitaja jina la kiongozi mmoja wa juu Azam) na wameonyesha nia ya kumuhitaji kweli kweli, tutazungumza nao kabla ya Ijumaa, bodi ya Azam imeenda kujadiliana,” alisema Ghost ambaye pia aliwahi kuipeleka Harambee Stars katika fainali za Afrika (AFCON) mwaka 2004.
Aliongeza kwamba mbali na kuwa na ofa ya kwenda kufanya majaribio katika klabu ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini, Olunga yuko mbioni kwenda Ulaya kufanya majaribio.
“Na hata akisaini Azam, mkataba wake utakuwa wazi ili akitakiwa kwa majaribio Ulaya aende. Hata ofa ya Afrika Kusini tuliisimamisha kwa ajili ya kuangalia mipango ya Ulaya kwanza, kiwango chake si cha kucheza Afrika,” Ghost.
Aliongeza kwamba Olunga amebakiza miezi minne ya kuitumikia Gor Mahia ambayo anaichezea kwa mkopo akitokea Thika United ya Kenya.
Gor Mahia kwa sasa imemkataza Olunga kuzungumza na vyombo vya habari na kumtaka aelekeze nguvu na akili kwenye mashindano ya Kombe la Kagame ambapo timu yake leo itacheza mechi ya hatua ya nusu-fainali dhidi ya Al Khartoum National ya Sudan.
JAMBOLEO
Taasisi ya kupambana rushwa TAKUKURU imetangaza ukomo wa matumizi ya fedha za kugharamia shughuli za kampeni kwa nafasi ya Urais ni shilingi bilioni 5 tu. Wakati huo huo TAKUKURU imesema kuwa hivi sasa inakunjua makucha na kuwataarifu wagombea wote kutotumia njia chafu kwa ajili ya kupata madaraka.
Mkurugenzi wa TAKUKURU Edward Hosea amesema sharia ya gharama ya uchaguzi inamtaka mgombea nafasi ya Urais kutumia bilioni 5 tu katika kampeni.
Pia sharia hiyo inamtaka mgombea kutumia milioni 80 kwa jimbo kubwa na jimbo dogo milioni 50 na jimbo la kawaida milioni 30.
Alisema ni vyema vyama vya siasa kuwa na akaunti maalum ili mkaguzi na mthibiti wa hesabu za Serikali kufanya hesabu ili kuona kiasi cha fedha zilizotumika baada ya uchaguzi kukamilika.
Dk.Hosea alisema fedha hizo ni kwa ajili ya kuendeshea kampeni hivyo wasitumie nafasi hiyo kurubuni wananchi ili wapate uongozi.
MWANANCHI
Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam kimeitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kusimamia kwa makini uandikishaji wapigakura jijini hapa ili wakazi wote wapate fursa ya kuandikishwa, ndani ya muda uliopangwa.
Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Simba aliwaambia wanahabari jana kuwa ufanisi katika uandikishaji utasaidia kumaliza idadi kubwa ya wakazi ambao bado hawajaandikishwa hadi sasa.
“NEC inatakiwa kuwa makini kukamilisha uandikishaji kwa kuongeza mashine na watendaji ili wakazi wengi wa Dar es Salaam waandikishwe,” alisema. Simba alisema CCM haitatetereka na uamuzi wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuhamia Chadema.
Alisema uamuzi huo siyo wa kwanza, kwani Augustine Mrema aliwahi kuondoka CCM na kujiunga na upinzani.
Kauli ya kiongozi huyo imekuja siku moja tangu Lowassa na mkewe, Regina, waihame CCM na kujiunga na Chadema na kuahidi kuendelea na safari ya matumaini ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Lowassa alijiunga CCM kwa ridhaa yake, hakuna aliyemshurutisha na ametoka kwa ridhaa yake kwenda Chadema hakuna aliyemshurutisha. “CCM itabaki kuwa CCM zaidi ya hilo, lipi jipya?”
Simba alisema tishio kwamba Lowassa ataondoka na makada wengi wa chama hicho ni propaganda za kupuuzwa. Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema muda wa kuandikisha wapigakura utaongezwa baada ya kujua idadi ya watakaosalia ifikapo mwisho wa kujiandikisha Agosti 31.
“Kwa sasa hatuwezi kusema tutaongeza siku ngapi, lakini ikifika siku ya mwisho tutajua watu wangapi wamebaki na hapo ndipo tutaongeza muda au la,” Lubuva.
Alisema utaratibu wa kuanza uandikishaji kuanzia saa moja asubuhi hadi 12 jioni, unaweza kuongeza kasi ya uandikishaji na hivyo watakaosalia watapewa muda kulingana na idadi yao.
Licha ya NEC kutoa agizo kwa mawakala wa BVR kuanza kufungua vituo kuanzia saa moja asubuhi, badala ya saa mbili, baadhi ya mawakala katika vituo wamekaidi agizo hilo.
Hata hivyo, agizo hilo lilionekana kupuuzwa na mawakala wa baadhi ya vituo ambao walifungua vituo hivyo kati ya saa mbili na saa tatu asubuhi. Siku zote bahati yako iko mikononi mwako tu, ili kudhibitisha kuwa ni kweli bofya kwenye picha iliyopo hapa chini.
Post a Comment