SHIRIKA
la Kutetea Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa limeitaka Nigeria
kuwasaidia kuavya mimba wanawake na wasichana waliopata ujauzito
walipokuwa wametekwa nyara na wapiganaji wa Boko Haram.
Shirika
la Amnesty International linakadiria kuwa zaidi ya wanawake na
wasichana 2,000 walitekwa nyara kaskazini-mashariki mwa Nigeria tangu
mwaka wa 2014, wakiwemo wanafunzi 276 waliochukuliwa shuleni na kundi la
Boko Haram katika eneo la Chibok.
“Wanawake
na wasichana hao walidhulumiwa kingono na wapiganaji wa Boko Haram
walipokuwa wametekwa nyara kwa miezi kadha na hata zaidi ya mwaka mmoja.
Wengi wao walilazimishwa kuolewa huku baadhi yao wakibakwa,” akasema
Zeid Ra’ad Al Hussein wa Baraza la Kutetea Haki za Kibinadamu la Umoja
wa Mataifa.
“Baadhi
ya waathiriwa waliookolewa kutoka mikononi mwa Boko Haram ni wajawazito
na wengi wao wanataka wasaidiwe na serikali kuavya mimba hizo. Lakini
nchini Nigeria, uavyaji mimba huruhusiwa tu endapo maisha ya mwanamke
yapo hatarini. Iwapo mimba hizo hazitatamatishwa zitaendelea
kuwakumbusha waathiriwa machungu waliyopitia mikononi mwa Boko Haram,”
akasema.
Hussein
aliitaka serikali kuingilia kati kuwasaidia wanawake na wasichana hao
kuavya mimba huku akionya kuwa huenda baadhi yao wakajitia kitanzi
kutokana na mimba hizo.
“Katiba
inafaa kufasiriwa vyema ili kujumuisha hatari kama vile kujinyonga na
maradhi ya kiakili kama masuala yanayoweza kulazimu uavyaji wa mimba,”
akasema.
Kadhalika,
Hussein aliitaka serikali kuhakikisha kuwa wasichana waliookolewa
kutoka katika ngome ya Boko Haram wanasaidiwa kutangamana na jamii zao.
Maafa kupindukia
Kundi la Kiislamu la Boko Haram limesababisha maafa ya zaidi ya watu 15,000 nchini Nigeria tangu mwaka wa 2009.
Kwingineko,
washambuliaji wawili wa kujitoa mhanga walifariki huku watu wengine
watatu wakijeruhiwa baada ya kujilipua karibu na hospitali katika mji wa
Maiduguri, Jumatano.
Washambuliaji
hao walijilipua dakika chache baada ya Makamu wa Rais Yemi Osinbajo
kuwasili mjini humo kwa ajili ya kutembelea kambi za wakimbizi ambao
wamekuwa wakitoroka mashambulio ya Boko Haram.
Shambulio
hilo lilitokea katika eneo ambapo wapiganaji wa kujitoa mhanga
walijilipua Jumamosi na kusababisha vifo vya watu watatu huku wengine 16
wakijeruhiwa.
Mji
wa Maiduguri umekuwa ukilengwa mara kwa mara na Boko Haram tangu Rais
Muhammadu Buhari, kuchukua hatamu za uongozi wa nchi hiyo mnamo Mei 29.
Rais Buhari alihamisha kituo cha kuelekeza operesheni dhidi ya Boko Haram kutoka Abuja hadi Maiduguri.
Hata hivyo, bado haijulikani ikiwa washambuliaji hao wa kujitoa mhanga wamekuwa wakilenga hospitali au la.
Post a Comment