Kifungu cha 112 ( 1 ) na ( 2 ) cha Sheria ya Mwenendo wa Kesi za Jinai kinaeleza kwa urefu kuhusu hati ya kumkamata raia ( warrant of arrest ) ambayo hutolewa na mahakama.
Kifungu hiki kimeeleza namna hati hii inavyopaswa kuwa na maudhui yanayopaswa kuwa ndani ya hati hiyo. Lengo ni kumfanya raia ajue anakamatwa na nani , kwanini na anapelekwa wapi. Ni hati ambayo imebeba taarifa zinazolenga kusimamia na kulinda haki za mtuhumiwa.
Yumkini mengi yaliyo katika hati hii huwa hayatekelezwi na wahusika. Raia wajue kuwa amri ya kukamatwa kwa mtu inapotolewa na mahakama ni lazima askari anayekuja kukamata awe na hati hii.
Asije askari kukukamata kwa maelezo kuwa ametumwa na mahakama wakati akiwa hana hati hii. Nisisitize tena kuwa amri ya kumkamata raia inapotolewa na mahakama mkamataji askari lazima aje na hati hii kwa ajili ya kutekeleza kazi hiyo. Na ili hati iwe halali lazima iwe na taarifa zifuatazo kama tutakavyoona hapa chini.
1. HATI LAZIMA IWE NA TARIFA HIZI.
( A ) LAZIMA HATI YA KUKAMATA IANDIKWE NA JAJI AU HAKIMU.
Upo utaratibu ambao umezoeleka ambapo makarani wa mahakama huandika hizi hati.
Hili ni kosa kubwa kwani kifungu hichohicho cha 112 cha Sheria ya Mwenendo wa Kesi za Jinai kimeweka wazi kuwa hati ya kukamata ni lazima iandaliwe na hakimu au jaji.
Afisa yeyote wa mahakama ambaye si hakimu au jaji hana kabisa mamlaka ya kuandaa hati hiyo.
Basi kama ndio hivyo ieleweke kuwa hati yoyote ambayo haikuandaliwa na hakimu au jaji ndio hati batili na ukamataji unaotokana na hati hiyo ni ukamataji haramu.
Nimeeleza katika makala zilizopita kuwa sheria inamruhusu raia kugomea ukamataji ambao ni haramu kama huo.
Hivyo niseme tena kuwa ikiwa hati ya kukamata haikuandaliwa na hakimu au jaji basi raia anayo haki ya kugomea kukamatwa.
( B ) LAZIMA HATI YA KUKAMATA IWE NA MUHURI WA JAJI AU HAKIMU .
Kawaida kila mahakama ina muhuri wake ambao huwa na utambulisho wa Mahakama husika. Muhuri huo huwa nao jaji au hakimu wa mahakama husika.
Muhuri huo ndio unaotakiwa kuwa katika hati ya kukamata. Kama ni hati imetolewa na mahakama kuu muhuri uoneshe kuwa ni wa mahakama kuu halikadhalika mahakama nyinginezo kama za wilaya na mwanzo.
( C ) HATI YA KUKAMATA LAZIMA IONESHE KOSA LA MTUHUMIWA KWA UFUPI.
Mpaka hati inatolewa kunakuwa na kosa ambalo tayari raia ametuhumiwa nalo. Hati hii haiwezi kutolewa iwapo hakuna kosa ambalo limeanzishwa.
Kutokana na hilo ni lazima kosa hilo lioneshwe ndani ya hati hiyo ili mtuhumiwa ajue anakamatwa kwa ajili ya nini ili naye ajue anaandaa nini na nini kuhusu kosa hilo.
Kwa mfano kosa liandikwe hivi, KUUA KWA KUKUSUDIA KINYUME NA KIFUNGU 196 CHA KANUNI ZA ADHABU.
( D ) LAZIMA HATI IONESHE JINA LA MTUHUMIWA AU WASIFU WAKE.
Isiwe hati imetolewa kwa ajili ya JOHN ikatumika kumkamata CLEMENT.
Aliyeandikwa kwenye hati ndiye huyohuyo anayepaswa kukamatwa. Hii ndio sababu ya hati hiyo kuwa na jina.
Kama haina jina basi iwe inachambua wasifu wa mlengwa kwa namna hivyo hivyo alivyo. Kama haina jina au wasifu wa mlengwa basi hati hiyo sio halali na mtuhumiwa anaweza kuigomea.
( E ) LAZIMA ITAJE JINA LA ASKARI/AFISA ALIYETUMWA KUKAMATA .
Si kila askari anamkamata anayemtaka. Hati ya kukamatwa hueleza askari/afisa maalum aliyepewa wajibu wa kukamata mhusika. Itamtaja kwa jina kuwa huyu ndiye aliyepewa mamlaka ya kumkamata fulani.
Haya yote ni kwa mujibu wa kifungu cha 112 ( 1 ) ( 2 ) cha Sheria ya Mwenendo wa Kesi za Jinai.
ACHA KUNYANYASWA, CHUKUA HATUA.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241
Siku zote bahati yako iko mikononi mwako tu, ili kudhibitisha kuwa ni kweli bofya kwenye picha iliyopo hapa chini.
Post a Comment