Hatimaye ameingia Chadema. Ilianza kama uvumi lakini jana ilikuwa dhahiri baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kutangaza rasmi kukihama chama tawala, CCM na kujiunga na Ukawa kupitia Chadema, huku akisisitiza; “Sasa basi, imetosha.”
Baada ya kukabidhiwa kadi ya Chadema na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe,
Lowassa alisema amejiunga na chama hicho kikuu cha upinzani ili
kutekeleza azma yake ya kuwakomboa Watanzania na kuendeleza safari ya
matumaini kupitia Ukawa.
“CCM kimepotoka, kimepoteza mwelekeo na sifa za kuendelea kuiongoza Tanzania,” alisema Lowassa katika mkutano wa kumkaribisha Chadema uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Ledger Bahari Beach na kurushwa moja kwa moja na vituo kadhaa vya televisheni na redio.
Dakika chache baada ya mkutano huo, CCM
kupitia mitandao yake ya kijamii ilitangaza kuitisha mkutano wa
wanahabari leo mchana kutoa taarifa muhimu, ikiaminika kuwa utakuwa wa
kumjibu kiongozi huyo.
Katika mkutano huo, Lowassa alitumia
dakika 13 kueleza sababu za kujiunga Chadema, mbele ya wenyeviti wenza
wa vyama vinavyounda Ukawa; Mbowe, Dk Emmanuel Makaidi (NLD), James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Prof. Ibrahim Lipumba (CUF).
Katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, Naibu wake (Bara), John Mnyika, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu hawakuonekana na hawakupatikana kuzungumzia sababu za kutokuwapo katika tukio hilo muhimu.
Lowassa ambaye aliingia katika ukumbi huo saa 10.20 jioni akiwa ameambatana na mkewe, Regina,
watoto wake, ndugu na jamaa, pia aligusia sakata la kampuni ya kufua
umeme ya Richmond lililosababisha ajiuzulu wadhifa wa waziri mkuu mwaka
2008, kwamba alifanya hivyo kwa manufaa ya nchi na alishindwa kuvunja
mkataba huo kutokana na amri kutoka mamlaka ya juu.
Wakati Lowassa akizungumza, wanachama wa Chadema walikuwa wakiitikia ‘peoples power’, na alipomaliza hotuba yake wanachama wao waliimba wimbo maalumu kuwa wana imani naye, “Tuna imani na Lowaasaa, oya oya oyaa.”
Katika hotuba yake, Lowassa aligusia jinsi mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM ulivyogubikwa na mizengwe na kusisitiza: “Nimetumia
muda huu kutafakari kwa kina yaliyotokea Dodoma na hatima yangu katika
siasa nchini. Pamoja na yaliyotokea Dodoma azma yangu iko palepale ya
kuanza mchakamchaka wa maendeleo ya kuiondoa nchi katika umaskini.
“Najua
sote tumevunjika moyo kwa yaliyotokea Dodoma na mazingira yaliyopelekea
matokeo yale. Mchakato uligubikwa na mizengwe, ukiukwaji wa maadili,
uvunjaji wa katiba na taratibu za uchaguzi za CCM.”
“Sikutendewa
haki. Kwa mantiki hii nitakuwa mnafiki kama nitaendelea kujidanganya
mimi mwenyewe na umma wa Watanzania kwa kusema kuwa bado nina imani na
CCM…,
MWANANCHI
Siku moja baada ya tovuti ya Mwananchi kunukuu habari zilizoripotiwa
na Mtandao wa African Review, kuhusu mishahara ya marais wa Afrika na
kwingineko duniani, Ikulu imekanusha habari hizo ikisema si za kweli.
Bila kutaja mshahara wa rais ni kiasi gani, taarifa ya Ikulu
iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu juzi, ilisema
habari hizi siyo za kweli. Ni uongo na uzandiki. Ni uzushi mtupu na ni
uzushi wa hatari.
Taarifa ya Ikulu imeikariri ripoti hiyo ya Mtandao wa African Review
ikisema: “Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete
anashikilia nafasi ya tano miongoni mwa viongozi 38 wa Afrika wanaolipwa
mshahara mnono zaidi.
“… Kuwa Rais Kikwete analipwa Dola za Marekani 192,000 kwa mwaka,
ikiwa ni malipo ya Dola za Marekani 16,000 kwa mwezi… Mshahara wa Rais
kwa mwezi ama kwa mwaka haufikii na hata wala kukaribia kabisa kiwango
kinachotajwa na Gazeti la Mwananchi,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo
bila kutaja kiwango anacholipwa.
Taarifa hiyo iliendelea kusema: “Tangu Uhuru, mwaka 1961, Rais wa
Tanganyika na baadaye tangu mwaka 1964 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania amekuwa miongoni mwa viongozi wanaolipwa mishahara ya chini
kabisa duniani. Mshahara wa Rais wa Tanzania kwa mwezi ni wa chini kiasi
cha kwamba mshahara wake unazidiwa, tena kwa mbali na mishahara
wanayolipwa baadhi ya watendaji wakuu wa baadhi ya taasisi za umma
nchini.
“Ni jambo la kushangaza kwamba Gazeti la Mwananchi, linalochapishwa
hapa nchini, linaweza kupata kiasi cha uongo anacholipwa Rais wa
Tanzania katika mitandao ya nje badala ya kuuliza rasmi na kupewa majibu
sahihi kwa kujiingiza katika uzushi wa kupindua kiasi hiki.
“Gazeti la Mwananchi haliwezi kuwa na nia nyingine yoyote isipokuwa
nia ya kuwachochea wananchi na kuwajengea chuki dhidi ya Serikali yao na
kiongozi wao mkuu,” ilisema taarifa hiyo ya Ikulu.
Ilimaliza taarifa hiyo kwa kusema: “Ni matarajio yetu, kuwa Gazeti la
Mwananchi litafanya jitihada za makusudi, kama taaluma ya uandishi wa
habari inavyoelekeza, kutafuta usahihi wa jambo hili na kuwaambia
Watanzania ukweli.”
HABARILEO
Taasis ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Singida inamhoji Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba kuhusiana na tuhuma za kukiuka Sheria ya gharama za Uchaguzi na Sheria za Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini.
Hatua hiyo imekuja siku chache tu baada
ya wagombea ubunge watatu kati ya wanne wanaogombea jimbo la Iramba,
mkoani hapa kugomea mchakato wa kampeni kuelekea kura za maoni wakidai
baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Siasa walikuwa wakimbeba mgombea mwenzao,
Mwigulu Nchemba.
Wagombea waliogomea zoezi hilo ni Juma
Killimbah, David Jairo na Amon Gyunda ambao walisema waliamua kuchukua
hatua hiyo kutokana na msimamizi wa uchaguzi kura za maoni CCM katika
jimbo hilo, Mathias Shidagisha na msaidizi wake, Mwita Raphael, kubariki
wao kuchezewa rafu na Nchemba.
Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Singida Joshua Msuya
alisema kuwa Nchemba anahojiwa kutokana na madai ya kukiuka makatazo
mbalimbali yaliyoainishwa kwenye Sheria za Kuzuia na Kupambana na Rushwa
namba 11 ya mwaka 2007.
Alisema kuwa makatazo hayo yanajumuisha
vitendo vyote vinavyokiuka sheria hiyo kabla ya kampeni, wakati wa
kampeni na baada ya kampeni ambapo baada ya uchunguzi wa kutosha
kukamilika jalada husika hupelekwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kwa
uamuzi wa mwisho.
Kutokana na malalamiko mbalimbali
kuifikia ofisi ya TAKUKURU, Msuya ametoa tahadhari kwa wagombea wote wa
udiwani na ubunge mkoani hapa kutojihusisha na vitendo vyovyote
vinavyoashiria kushawishi wanachama kuwachagua vinginevyo wakigundulika
hatua kali dhidi yao zitachukuliwa.
Wakati kampeni zinaendelea kwenye
majimbo mbalimbali mkoani hapa, vitendo vya ukiukwaji wa Sheria ya
gharama za Uchaguzi vimekuwa vikiripotiwa kwa wingi kuliko wakati
mwingine wowote wa kipindi cha uchaguzi.
Aidha, inaripotiwa kuwa hali si shwari
katika jimbo la Mkalama kutokana na baadhi ya wagombea wenye uwezo
kifedha kudaiwa kumwaga fedha na zawadi mbalimbali kwa wanachama na
wananchi wa kawaida ili wagombea hao waweze kuwachagua siku ya kura za
maoni itakapofika.
MWANANCHI
Hayawi hayawi sasa yamekuwa. Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa
ameweka rekodi ya kuwa kada wa kwanza aliyewahi kushika nafasi ya
waziri mkuu kukihama chama tawala, CCM na kujiunga na upinzani.
Katika orodha ya mawaziri wakuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
tangu uhuru, Lowassa ni waziri mkuu wa tisa kushika madaraka hayo.
Alishika wadhifa huo kuanzia Desemba 30, 2005 hadi Februari 7, 2008.
Makada wengine wa CCM waliowahi kushika wadhifa wa waziri mkuu ni, Julius
Nyerere, Rashidi Kawawa, Edward Sokoine, Cleopa Msuya, Dk Salim Ahmed
Salim, Joseph Warioba, John Malecela, Frederick Sumaye na Mizengo Pinda.
Lowassa ni kati ya mawaziri watatu waliowahi kuwania urais mara mbili
na kushindwa. Wengine ni Malecela (1995 na 2005), Sumaye (2005 na
2015). Mbunge huyo wa Monduli aliyejitokeza 1995 na 2015 na ambaye
amekuwa akisononeka namna mchakato wa kupata mgombea ulivyoendeshwa,
ameamua kuhamia upinzani ili kuweka haki ndoto ya safari yake ya
matumaini.
Katika kipindi cha wiki tatu sasa, kumekuwapo minong’ono ndani na nje
ya CCM na kwenye mitandao ya kijamii, kwamba nchi itatikisika kutokana
na fununu za Lowassa kuhamia upinzani.
Kulikuwapo kila aina ya propaganda za kubeza hatua hiyo na nyingine
zikipongeza na kutahadharisha kuwa, kama angehamia upinzani, ungekuwa
mwisho wa CCM.
Tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, mawaziri wakuu sita
wamewahi kuomba kuteuliwa na CCM kupeperusha bendera ya urais na
kushindwa, lakini hakuna aliyethubutu kuhama chama hicho tawala.
Mwaka huu, Lowassa alijitosa kwa mara ya pili kuwania urais,
akiungana na makada wengine 37 wa CCM waliorudisha fomu wakiwamo Sumaye
na Pinda.
Majina ya Lowassa na mawaziri wakuu wenzake hayakupenya hata Tano
Bora, yaliishia katika Kamati ya Maadili. Wajumbe watatu wa Kamati Kuu
walifichua kile walichodai ukiukwaji mkubwa wa kanuni kwani kamati
iliyopaswa kuchuja majina ni Kamati Kuu na siyo Kamati ya Maadili.
Dk Emanuel Nchimbi ambaye amekuwa mjumbe wa CC kwa miaka 17, Sophia
Simba na Adam Kimbisa, walitangaza rasmi kujiweka kando na maamuzi hayo
ya Kamati Kuu.
HABARILEO
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala,
imewataka wafanyabiashara waliojenga vibanda vyao katika eneo la
Jangwani, kuvibomoa vibanda hivyo mara moja kabla ya kesho kwa kuwa
wamekiuka utaratibu kwa kujenga eneo hatarishi.
Aidha Manispaa hiyo imesema endapo muda
waliotoa ukifika agizo hilo likiwa halijatekelezwa watapitisha
tingatinga eneo hilo kwa ajili ya kubomoa vibanda hivyo na kisha
kuwachukulia hatua wahusika kwa kufanya uvamizi.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi
alisema lengo lao lilikuwa ni kuwasaidia wafanyabiashara wanaopanga
bidhaa zao barabarani lakini sasa wapo watu waliovamia eneo hilo na
kujenga vibanda.
“Tunatangazia
wavamizi hao wabomoe mara moja na baada ya hapo kama agizo
halitatekelezwa tutabomoa na tutawashitaki kwa uvamizi… Naomba muelewe
kwamba Manispaa ya Ilala haijatoa eneo la kujengwa.”
“Ardhi
yote iliyopo Manispaa inasimamiwa na Manispaa lakini hakuna mtu
aliyejenga katika eneo la Jangwani aliyepewa kibali na Manispaa… Nia
ilikuwa kuwasaidia wafanyabiashara wanaotandika bidhaa zao chini ila kwa
sasa waliopo pale si wahusika bali ni wavamizi kwa kuwa wanaotandika
bidhaa hadi leo wapo mitaani.”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Isaya Mngurumi
alisema walishatamka kwamba eneo hilo haliruhusiwi kujengwa kibanda na
waligawa kwa wale wanaotembeza vitu mkononi ili wafanye kama gulio kwa
kupanga bidhaa zao chini.
“Lile
ni eneo hatarishi kwa ajili ya ujenzi wa kudumu, hivyo likitumika kama
gulio kwa kumwaga bidhaa chini, kipindi cha mvua watasitisha biashara
lakini waliojenga hawakufuata utaratibu na tunawataka wabomoe mara
moja,” alisema.
Siku zote bahati yako iko mikononi mwako tu, ili kudhibitisha kuwa ni kweli bofya kwenye picha iliyopo hapa chini.
Post a Comment