Kada mpya wa Chadema, Edward Lowassa
jana amerejesha fomu ya kuwania urais, huku akifanikiwa kupata
wadhamini milioni 1.6, zaidi ya nusu ya kura za urais ambazo chama hicho
kilipata kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
Naibu katibu mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu
alisema idadi hiyo ya wadhamini inaashiria ushindi wa kishindo, kwa
maelezo kuwa inakaribia idadi ya kura alizopigiwa katibu mkuu wa chama
hicho, Dk Willibrod Slaa alipogombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2010.
Katika Uchaguzi huo, Dk Slaa alishika
nafasi ya pili baada ya kupata kura 2,271,941 sawa na asilimia 26.34,
huku Rais Jakaya Kikwete akipata kura 5,276,827 sawa na asilimia 61.17. Lowassa alipochukua fomu za kuomba
kuteuliwa kuwania urais kwa tiketi ya CCM, kabla ya kuhamia Chadema,
alidhaminiwa na wanachama 870,000 nchi nzima.
Dk Slaa, ambaye hajaonekana hadharani
tangu Lowassa ajiunge Chadema, jana hakuwapo kwenye ofisi za chama hicho
wakati mbunge huyo wa Monduli alipokuwa akirejesha fomu. Hakuna kiongozi aliyekuwa tayari kuzungumzia suala lake, lakini baadhi ya maofisa wa Chadema walisema wanaendelea kuchapa kazi.
Kama ilivyokuwa juzi katika hafla fupi
wakati Lowassa akichukua fomu, umati mkubwa ulifurika na kusababisha
Mtaa wa Ufipa uliopo Wilaya ya Kinondoni kufungwa, watu walijazana tena
na safari hii umati huo ukiwa umebeba mabango ya kumsifu Waziri Mkuu
huyo wa zamani.
Katika hafla ya jana, makamu mwenyekiti
wa Chadema-Bara, Profesa Abdallah Safari alieleza jinsi Chadema
ilivyojipanga kuchukua nchi na siyo kushinda ubunge na udiwani pekee na
kwamba Lowassa amebakiza hatua mbili tu kuingia Ikulu, jambo walilodai
kuwa limeichanganya CCM.
Wakati Lowassa ambaye alitangaza rasmi
kujiondoa CCM na kujiunga na Chadema Julai 28 mwaka huu akisubiri
kupitishwa na Mkutano Mkuu wa chama hicho utakaofanyika Agosti 4, habari
za ndani zinaeleza kuwa vigogo kadhaa wa CCM watatambulishwa katika
mkutano huo.
Habari hizo zinaeleza watakaotambulishwa
siku hiyo ni wenyeviti wa CCM wa mikoa, wilaya na waliokuwa wabunge wa
chama hicho ambao wanamuunga mkono Lowassa.
Jana Lowassa, aliyekuwa amevaa shati
jeupe na suruali nyeusi na aliyekuwa katika gari aina ya Toyota Land
Cruiser VX, alifika makao makuu ya Chadema saa 9:35 alasiri akiwa pamoja
na familia yake na alipokewa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wamebeba
mabango yenye ujumbe mbalimbali.
Baadhi ya ujumbe huo ni “Chini ya
Lowassa umaskini haupo”, “Kwa Lowassa hata maskini atapata ajira” na
“Kingunge Ngombare-Mwiru karibu Ukawa”. Kingunge ni kada mkongwe wa CCM
na anamuunga mkono Lowassa.
Mbali na kubeba mabango, watu hao
walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za kumsifu Lowassa na kushangilia
pale ilipokuwa ikitajwa mikakati ya chama hicho kushika dola.
Akieleza taratibu na kanuni za kudhamini
mgombea urais, mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa chama hicho,
Benson Kigaira alisema mgombea urais anatakiwa kudhaminiwa na wanachama
wasiopungua 200.
“Naamini
fomu za Lowassa zitakuwa na idadi hiyo ya wadhamini. Ila baada ya
mgombea kuchukua fomu jioni yake wanachama wa Chadema, wapenzi na
Watanzania walifurika katika ofisi za Kanda, mikoa na majimbo nchi nzima
wakiomba kumdhamini,” Kigaira.
Alisema wanachama hao walidhani fomu
hizo zimepelekwa kila mkoa, kutokana na kuepuka kuwanyima fursa hiyo
chama hicho kilipeleka fomu ili wanachama wamdhamini na kupewa masharti
kuwa lazima wawe wamejiandikisha kupiga kura, wataje namba zao za simu.
Siku zote bahati yako iko mikononi mwako tu, ili kudhibitisha kuwa ni kweli bofya kwenye picha iliyopo hapa chini.
Post a Comment