Watu wa tano kutoka nchini Tanzania
miongoni mwao mmoja raia kutoka nchini Kenya wamethibitika kufariki
dunia kufuatia Mkanyagano uliotokea jana karibu na mji mtakatifu wa
kiislam Macca na kusababisha watu zaidi ya 717 kufariki dunia.
Mufti wa Tanzania Sheikh Abu Bakari Zuberi katika taarifa yake kwa
viombo vya habari amethibitisha kutokea vifo vya watu watano na
watanzania waliotambuliwa hadi jana usiku ni Bi Mwanaisha Hassan Juma,
Mkungwe Suleiman Hemedi na Sefu Saidi Kitimla.
Mwanamke mwingine mmoja Mtanzania jina halijaweza kupatikana hadi Alhamisi usiku wakati tukiandaa taarifa hii.
Raia wa Kenya ametambuliwa kwa jina la Bi Fatuma Mohammed Jama.
Kuna taarifa ya mahujaji wanawake wawili ambao hadi Alhamisi usiku
walikua hawajapatikana hivyo hatukua na uhakika juu ya usalama wao hadi
tutakapowaona ama kupata taarifa zao.
Ifahamike kuwa majina yamepatikana kupitia vitambulisho vyao
ambavyo wahanga wa tukio hili waliweza kuvichukua kutoka kwenye miili ya
marehemu.
Nimepokea taarifa za majeruhi miongoni mwa mahujaji wetu wa
Tanzania na baadhi ya majeruhi hao nimeonana nao mara baada ya
kuruhusiwa kutoka hospitalini.
Vilevile nimeagiza maafisa wetu wa Bakwata nilionao hapa Mina
kuendelea kufuatilia habari na taarifa za mahujaji wetu katika hospitali
na sehemu za kuhifadhia maiti.
Nimefanya hivyo ili niweze kuwa na uhakika juu ya usalama wa mahujaji wetu.
Katika kipindi hiki cha taharuki kubwa tunafanya mawasiliano na
wizara husika hapa Saudi Arabia kwa kushirikiana na serikali yetu
kupitia ubalozi wetu hapa Saudi Arabia. Natambua uwepo wa mkanganyiko wa
taarifa ambazo zinazidisha taharuki kwa ndugu na jamaa wa mahujaji
wetu.
Nachukua fursa hii kuwaomba ndugu na jamaa wa mahujaji kuwa watulivu na kuwa na subra katika wakati huu mgumu sana kwetu sote.
Tunaendelea kufuatilia kwa karibu sana na Insha Allah mara tu tukipata taarifa za uhakika basi tutawafahamisha.
Kutokana na idadi ya maiti kuwa kubwa serikali ya Saudi Arabia
wanaendelea na zoezi la kutambua uraia wa kila mwili ili waweze kutoa
taarifa tunatarajia wakati wowote tutakuwa tumepata taarifa zaidi.
Wabillahi Tawfiiq.
Sheikh Abu Bakari Zuberi
Mufti wa Tanzania.
Post a Comment