KUNA mtu mmoja matata sana ndani Yanga kwa sasa, Malimi Busungu. Huyu jamaa ametangaza hatari na kusisitiza kwamba yeyote atakayejiingiza kwenye anga zao kwa sasa amejiloga mwenyewe. Haponi.
Busungu ameenda mbali zaidi kwa kuwataja kwa majina kabisa watu ambao ni moto wa kuotea mbali ndani ya Yanga na ambao kila wakilala na kuamka wanaota mabao tu.
Straika huyo amefungua mdomo wake na pia kuzinyooshea vidole timu zote ambazo hazijakutana na kikosi chao akisema uwepo wa washambuliaji wenzake Amissi Tambwe, Donald Ngoma ni vigumu safu hiyo kutoka bila ushindi.
Akizungumza na Mwanaspoti mjini hapa, Busungu alisema kwa sasa anafurahia kucheza pamoja na washambuliaji hao ambao ubora wao tofauti ndiyo unaowafanya kutoka wakishangilia hata wakikutana na timu yoyote.
Busungu alisema Ngoma ni straika mzuri ambaye anajua kupambana na beki yeyote bila kuogopa huku Tambwe akiwa vyema katika kutumia nafasi endapo anasahaulika ambapo akiongezeka na yeye kazi ya kuwazuia inakuwa ngumu na kutamba watafunga sana.
Alisema ameanza kuzoea kucheza na wawili hao wa kigeni ambao wanampa nafasi kujua ajifiche wapi aweze kufunga hali ambayo itazidi kuipa pointi tatu Yanga katika kila mechi zijazo.
“Angalia nilivyofunga bao la kwanza(kwenye mechi ya Mtibwa) kazi kubwa aliifanya Ngoma kugombea mpira na yule beki wa Mtibwa nilijua kuna kitu kitatokea pale na kweli nikaupata mpira na kufunga kirahisi, Ngoma uzuri wake haogopi kitu anajua kupambana,” alisema Busungu.
“Watu wanaodhani tunabahatisha kama hatujakutana nao wataona Yanga tuko vizuri kupita maelezo, kwasasa tunataka kuhakikisha tunapata pointi tatu tu katika kila mchezo.”
YONDANI NOMA
Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm ameiangalia safu yake ya ulinzi na kusema vijana wako sawa, ila huyu Kelvin Yondani huyu sio wa kawaida lazima atakuwa amepitia jeshini.
Akizungumza na Mwanaspoti Pluijm alisema Yondani kwasasa anapitia kipindi kitamu cha kucheza akiwa katika ubora wake mkubwa ambapo kazi anayoifanya sasa katika kikosi hicho hajawahi kuiona tangu atue katika ardhi ya Tanzania.
Post a Comment