Zaidi ya familia mia moja hazina makazi wilayani Uvinza mkoani Kigoma.
Zaidi ya familia mia moja katika kijiji cha Kirando kata ya Sunuka wilayani Uvinza mkoani Kigoma hazina makazi baada ya nyumba zaidi ya hamsini walizokuwa wakiishi kuezuliwa na kubomoka kufuatia mvua kubwa iliyonyesha kwa masaa sita usiku ambayo pia imeleta uharibifu mkubwa wa mali.
Waathirika wa mafuriko hayo ambayo yameathiri wananchi katika vitongoji vya Kirando, Nyamamba na Nyankima wamesema kutokana na mvua hiyo kunyesha usiku hali ilikuwa ngumu kufanya uokoaji ambapo mali kadhaa ikiwa ni pamoja na vyakula vilisombwa na maji na kupelekwa ziwa Tanganyika hali ambayo imewaacha waathirika bila ya makazi, chakula na mahitaji muhimu ya kibinadamu.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Uvinza Mrisho Gambo akizungumza baada ya kuwatembelea waathirika wa tukio hilo ambao sasa wanahifadhiwa na majirani na katika majengo ya taasisi za umma kijijini hapo, amesema serikali inafanya tathmini na kutanza kutoa msaada wa haraka kutokana na wananchi hao kuhitaji msaada wa haraka kutokana na kushindwa kuokoa mali zao na kwamba katika tukio hilo hakuna mtu aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa.
Post a Comment