Wakati vyombo vya juu vya baadhi ya vyama vya siasa vikiwa vimeanza
hatua za mwisho za kupitisha wagombea wa ubunge na udiwani tayari kwa
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, hadi juzi wabunge 51 walikuwa wameanguka
kwenye kura za maoni za ndani ya vyama vyao.
Idadi hiyo ni takriban asilimia 14 ya wabunge 357 wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano, inayojumuisha waliochaguliwa na wananchi na wa viti
maalumu, ambao waliamua kwenda kupambana majimboni.
Miongoni mwa walioanguka ni mawaziri wa Serikali ya Muungano na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambao walikuwa wakitetea viti vyao
majimboni.
Kati ya wabunge hao walioanguka, wawili wanatoka Chadema, wanne CUF na wengine 45 waliosalia wanatoka CCM.
Matumaini pekee yaliyosalia kwa wabunge hao ambao baadhi yao wamekata
rufaa kupinga matokeo ya kura za maoni, ni huruma za vikao hivyo
ambavyo vinaweza kubadili matokeo ya baadhi ya majimbo, hasa ambayo
taratibu zilikiukwa na ushahidi wa kuwapo matumizi ya rushwa.
Wakati wabunge walioanguka Chadema wanasubiri kwa hamu kikao cha
Kamati Kuu kilichoanza juzi kupitia majina hayo, wa CCM wanasubiri
mfululizo wa vikao vinavyoanza leo hadi Agosti 13, wakati mchakato
kupitisha wagombea wa NCCR-Mageuzi bado.
Kwa wabunge wa CUF, hakuna matumaini kutokana na vikao vya juu vya chama hicho kukamilisha kazi yake hivi karibuni. Mbali na walioanguka, wabunge waliopita katika kura za maoni lakini
vyama vyao vinaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), nao
watalazimika kusubiri hadi vyombo hivyo vya mchujo vitakapomaliza kazi,
kujua kama wamepita.
Hiyo inatokana na makubaliano ndani ya umoja huo ya kusimamisha mgombea mmoja atakayeungwa mkono na vyama vyote.
Kwa mujibu wa makubaliano ya vyama hivyo vinne; Chadema, CUF, NLD na
NCCR – Mageuzi- kinachooonekana kina nguvu kwenye jimbo fulani ndicho
mgombea wake ataachiwa kupeperusha bendera ya umoja huo, jambo ambalo
vyama hivyo vilisema vimekamilisha kazi ya mgawanyo kwa asilimia 95.
Wakati Chadema, CUF, NCCR na NLD
wakisubiri utekelezwa wa makubaliano hayo, wabunge wa CCM watakuwa
njiapanda baada ya chama hicho kueleza kuwa hakitarudia makosa ya mwaka
2010 ya kupingana na maoni ya wanachama kwa kutengua matokeo ya kura za
maoni.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jamidu Katima alisema kuanguka kwa wabunge hao kunatokana na wengi wao kutoonekana majimboni baada ya kupewa dhamana ya kuongoza wananchi.
“Kama kiongozi umepewa dhamana, lakini huonekani jimboni basi ni
dhahiri wananchi watakukataa. Wakikuona unachukua fomu watakushangaa
lakini ujue watakukataa kwa sababu huwatatulii kero zao kama ulivyoahidi
awali.”
Profesa Katima alisema kwa sasa Watanzania wameamka, hivyo ni vigumu
kudanganyika na kwamba kama kiongozi hatumii vyema dhamana aliyopewa,
wananchi watamuacha apumzike kwa amani.
Maoni kama hayo yalitolewa na mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo
ambaye alisema zipo sababu chekwa za baadhi ya mawaziri kushindwa
kwenye kura za maoni, mojawapo ikiwa ni makundi na kushindwa kutimiza
ahadi.
Dk Makulilo alisema ni rahisi kwa wananchi kuacha kumchagua kiongozi
baada ya kuona hajatimiza kile alichoahidi hivyo wakaona wajaribu
kiongozi mwingine pengine atawatatulia kero zao. Kuhusu kuanguka kwa wanasiasa nguli wa CCM, mhadhiri huyo alisema
sababu nyingine ni siasa za makundi ambako kundi moja tu linaweza
kufanya juhudi ili mwingine ashindwe.
“Sasa hivi tunazungumzia mtu
kuanguka katika chama chake, kwa hiyo siasa za makundi ndani ya chama
hicho inaweza kusababisha kuanguka katika kura za maoni,” alisema. Sababu nyingine aliyoitaja Dk Makulilo ni wimbi la vijana na kuwa
inawezekana wananchi wanahamia kwa wanasiasa vijana zaidi baada ya kuona
wengine amekaa madarakani kwa muda mrefu.
Siku zote bahati yako iko mikononi mwako tu, ili kudhibitisha kuwa ni kweli bofya kwenye picha iliyopo hapa chini.
Post a Comment