Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kinatarajiwa kufanya hafla ya aina yake ya kumuenzi Rais Jakaya Kikwete. Kitamuenzi kama sehemu ya kutambua mchango wake wa hali na mali,
uliofanikisha kuanzishwa kwa chuo kikuu hicho cha aina yake Tanzania na
nje ya Tanzania.
Taarifa ya kusudio la chuo hicho kumuenzi Rais Kikwete, limetolewa mwishoni mwa wiki na Makamu Mkuu wa UDOM, Prof. Idris Kikula
wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mabalozi na Maofisa wa
Uwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa
Mataifa.
Profesa Kikula na ujumbe wake yuko katika ziara ya kikazi nchini
Marekani. Ziara hiyo ilimfikisha jijini New York, ambapo ujumbe ulipata
fursa ya kukagua vifaa tiba na vitabu vya kiada na ziada, ambavyo
vimetolewa na wadau mbalimbali wenye mapenzi mema na Tanzania.
Baada ya kukagua vifaa na vitabu hivyo na kujiridhisha, Makamu Mkuu
wa UDOM ameushukuru Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwa kuwapatia fursa
hiyo ya kujionea wenyewe aina ya vifaatiba na vitabu, ambayo amesema
vitakuwa msaada mkubwa kwa Kitivo cha Sayansi ya Afya cha Chuo hicho.
“Waheshimiwa Mabalozi, mimi na
ujumbe wangu napenda kwa moyo wa dhati kabisa kutoa shukrani zetu kwa
kutuonesha vifaa na vitabu ambavyo kupitia kwenu wafadhili wamevitoa
kuwasaidia watanzania nanyi mkaona bora kutushirikisha na kuona namna
gani chuo chetu kinaweza kunufaika na misaada ya aina hii,” Profesa Kikula.
Aliongeza kuwa Kitivo cha Sayansi ya Afya na ambacho pia kina
zahanati, kinahitaji sana misaada ya kila aina ili kiweze kutimiza lengo
lake kuu la kuwaandaa madaktari na wataalamu mbalimbali, lakini pia
kutoa huduma uchunguzi na matibabu siyo tu kwa wanafunzi na wafanyakazi
wa UDOM bali pia kwa Watanzania wote.
“Uongozi wangu unapenda
kutambua juhudi zenu hizi za kushirikiana na wadau mbalimbali kusaidia
siyo tu vyuo vikuu vyetu, lakini na watanzania. Mmedhihirisha kwa
vitendo na si maneno na hii imetupa faraja sana na kudhihirisha namna
gani tunaweza kushirikiana kwa karibu zaidi.”
Alisema kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dodoma ni ndoto na hatimaye
mbegu iliyopandwa na Rais Kikwete, ndoto uliyoanzia kwenye kampeni yake
ya urais mwaka 2005.“Ilianza kama ahadi ya kampeni, ahadi ambayo haikuishia katika maneno
matupu ya ahadi bali aliitekeleza ahadi ile na leo hii tunaiona mbegu
aliyoipanda ikichanua na mavuno yanaonekana,” alisema Prof. Kikula kwa
msisitizo wa aina yake.
Anasema haikuwa rahisi kuifanikisha ndoto ya Rais kutokana na pingamizi mbalimbali kutoka nje na ndani ya serikali. Balozi Tuvako Manongi, Mwakilishi wa Kudumu wa
Tanzania katika Umoja wa Mataifa, ameushukuru uongozi wa UDOM kwa
kuitikia mwito wa Uwakilishi wa kutumia ziara yao ya kikazi, kujionea
kukagua vifaa na vitabu ambavyo vimepatikana kwa ushirikiano wa
uwakilishi na wadau mbalimbali.
Siku zote bahati yako iko mikononi mwako tu, ili kudhibitisha kuwa ni kweli bofya kwenye picha iliyopo hapa chini.
Post a Comment