Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohammed Othman Chande
amesema kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kufanya uteuzi wa mara kwa mara
wa majaji nchini, kimeongezea kwa kiasi kikubwa utendaji wa Idara ya
Mahakama na hadi sasa kuna Majaji takribani 100, jambo ambalo halijawahi
kutokea miaka ya nyuma.
Aidha, ameahidi kutokana na wingi wao, sasa wana uhakika wa kuongeza
uchapaji kazi na kwa kuanzia, wameweka lengo kwamba, kesi zote katika
Mahakama Kuu na Mahakama ya Biashara zisiendeshwe zaidi ya miezi 10.
Jaji Chande alikuwa akizungumza na waandishi wa habari Ikulu, Dar es
Salaam jana mara baada ya Rais Kikwete kuapisha Majaji wa Mahakama Kuu
13 na Jaji mmoja wa Mahakama ya Rufani. “Tunamshukuru
Rais kwa ongezeko hili la majaji ambalo sasa linaifanya Tanzania kuwa
na majaji 100, hawa ni wengi haijawahi kutokea,” alisisitiza.
Alisema ongezeko hilo, litasaidia sekta hiyo kushughulikia tatizo la
mlundikano wa kesi hasa katika kanda za Mahakama Kuu, ambazo kwa muda
mrefu zimekuwa zikielemewa na kesi nyingi.
Alitaja kanda ambazo zina mzigo wa kesi nyingi, ambazo sasa
zitapunguziwa mzigo huo kutokana na ongezeko hilo la majaji kuwa ni
Kanda ya Mahakama Kuu ya Bukoba, ambayo Jaji mmoja alikuwa
akishughulikia kesi 3,000 na Mwanza jaji mmoja kesi 600.
Aidha, alisema ongezeko hilo litasaidia maeneo mengine yenye kesi
nyingi pia, ambayo ni Tabora na vitengo vya Mahakama Kuu kama vile Idara
ya kazi, Ardhi na Biashara. Alisema tayari sekta ya Mahakama
ilishajiwekea mikakati ya kushughulikia changamoto zinazoikabili sekta
hiyo, ikiwa ni pamoja na kubadilisha ratiba, ambapo kwa upande wa Majaji
walipangiwa Jaji mmoja sasa kusikiliza kesi 220, Hakimu Mkazi wa wilaya
na Mkoa kesi 250 na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo kesi 260.
“Kila Mahakama pia imewekewa malengo yake na lengo kubwa ni
kuhakikisha kesi hazichukui muda mrefu kusikilizwa, kwa mfano kwa mujibu
wa mabadiliko haya kitengo cha Biashara cha Mahakama Kuu kesi zake
hazitosikilizwa kwa muda wa zaidi ya miezi 10 hadi mwaka mmoja,”
alisisitiza.
Aliwataka majaji walioteuliwa na kuapishwa jana kutambua kuwa
waliteuliwa katika nyadhifa hizo, kutokana na utendaji, uzoefu na
uadilifu wao, hivyo wanapaswa kuhakikisha wanadumisha sifa hizo katika
utendaji wao.
Alisema kabla ya majaji hao hawajaanza rasmi kazi, wataandaliwa
mafunzo maalum ili waweze kuendana na utaratibu wa kimahakama kwa kuwa
kati ya majaji hao, watano walikuwa mawakili wa kujitegemea, watano
mawakili wa Serikali na watano walikuwa mahakamani.
Akizungumzia suala la uchaguzi, Chande, alisema tayari wamejipanga
kuhakikisha kuwa kesi za uchaguzi zinasikilizwa kwa haki na muda ambapo
hazitosikilizwa kwa zaidi ya miezi sita.
Kuhusu Majaji waliotuhumiwa kupatiwa mgawo wa fedha za akaunti ya
Escrow, alisema tume iliyoundwa kufanya uchunguzi na upelelezi, tayari
imekamisha upelelezi wake wa awali na itakapokamilisha kuuandaa,
itaukabidhi rasmi kwa mamlaka ya uteuzi (Rais) kwa hatua zaidi.
Majaji hao ni Profesa Eudes Ruhangisa anayedaiwa kupata Sh milioni
400.25 na Aloysius Mujulizi Sh milioni 40.4. Awali, akizungumza na
gazeti hili kuhusu uteuzi wake, Jaji wa Mahakama Kuu Ignas Kitusi,
alisema kuna mipango mingi ya kuboresha huduma za Mahakama, ambapo
aliahidi pamoja na wenzake kutekeleza mipango hiyo ikiwemo kurejesha
imani ya wananchi dhidi ya Mahakama ambayo kwa sasa imepotea.
Siku zote bahati yako iko mikononi mwako tu, ili kudhibitisha kuwa ni kweli bofya kwenye picha iliyopo hapa chini.
Post a Comment