Wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) jana walimbana Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Prof. Ibrahim Lipumba wakimtaka kueleza ukweli juu ya taarifa zinazodai kuwa amejiuzulu wadhifa huo.
Wanachama hao walifika asubuhi na kukusanyika katika Ofisi za Makao
Makuu ya CUF Buguruni, Dar es Salaam, kwa lengo la kujua hatma ya
kiongozi wao huyo. Walipofika hapo, alikuwa na kikao kirefu na wazee na
viongozi wa dini kuhusu kile alichotaka kukieleza mbele ya vyombo vya
habari. Baada ya kuwepo kwa kelele nyingi na za muda mrefu, zilizokuwa
zikipigwa na wanachama hao zaidi ya 200, waliokuwa wakiimba nyimbo
mbalimbali, ilimlazimu Profesa Lipumba kutoka ofisini kwake na
kuwatuliza.
Hata hivyo, wanachama hao waliendelea kubaki na sintofahamu kutokana
na yale aliyowaambia. Lipumba aliwataka wanachama hao, kuielewa vizuri
Katiba ya CUF, kwa kuwa chama hicho kinaendeshwa kwa kufuata Katiba.
Alieleza kuwa kila mwanachama kwa nafasi yake, anatakiwa kukijenga chama
hicho.
“Mwaka 1995 nilikuwa ni mwanachama wa kawaida na niliteuliwa kuwa
mgombea urais. Chama chetu ni taasisi, tena kubwa na sio mtu mmoja,
hivyo tujenge chama chetu kama taasisi,” alisema Profesa Lipumba kisha
kurudi ofisini kwake.
Hata hivyo, wanachama hao waliendelea kupiga kelele za kutaka
ufafanuzi wa kauli hiyo, ambayo wengi walidai kuwa haijaeleweka
inamaanisha nini. Mmoja wa viongozi wa dini, aliyejitambulisha kuwa ni
Mchungaji Godfrey Sombi alisema hali si shwari, kwani Profesa Lipumba
anataka kubaki mwanachama wa kawaida ndani ya chama hicho.
Mchungaji Sombi alisema sababu kubwa ni kutokana na baadhi ya
viongozi wa Umoja wa vyama vinne vya upinzani (Ukawa), ambao chama hicho
ni miongoni mwa vinavyounda umoja huo, kuvunja malengo yake.
“Hajaridhishwa na ujio wa Lowassa (Edward) ndani ya Ukawa na kupewa
nafasi ya kupeperusha bendera kwa nafasi ya urais, kwa hiyo anataka
kubaki kuwa mwanachama wa kawaida,” alisema kiongozi huyo wa dini.
Lowassa amejiunga na Ukawa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) wiki moja iliyopita na juzi aliteuliwa kuwa mgombea urais wa
chama hicho na umoja huo, wenye vyama vinne vya Chadema, CUF,
NCCR-Mageuzi na NLD.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, baadhi ya wanachama
wa CUF walimtaka Profesa Lipumba kuweka wazi kuhusu taarifa zinaripotiwa
na vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Walitaka Profesa huyo maarufu wa Uchumi na aliyegombea urais mara nne
tangu mwaka 1995, aendelee kuwa kiongozi wao, kwani wana imani naye.
Abdallah Simba alisema kauli iliyotolewa na Profesa Lipumba, bado
imewafumba macho, kwani hawaelewi ukweli wa taarifa za kujiuzulu na
walitegemea angetoa taarifa za kukanusha kujiuzulu ndani ya chama hicho
au kueleza kinachoendelea.
Juzi hakuwapo wakati Lowassa akipitishwa na Mkutano Mkuu wa Chadema
kuwa mgombea urais pamoja na Mgombea Mwenza, Juma Duni Haji ambaye
alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF Zanzibar na sasa amehamia Chadema.
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad alihudhuria mkutano
huo, uliofanyika Dar es Salaam na alitangazwa kuwa Mgombea wa Urais wa
Ukawa kwa Zanzibar.
Post a Comment